WAZIRI WA KILIMO, MALIASILI, MIFUGO NA UVUVI AZINDUA BODI TATU-July 2017


Waziri wa kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Mhe. Hamad Rashid Mohamed amesema madhumuni ya kuazishwa kwa bodi ya kampuni ya uvuvi ya Zanzibar (ZAFICO) ni kuimarisha miundombinu na kuendeleza Uvuvi kibiashara, pamoja na kuazisha viwanda vya samaki nchini. Uwepo wa kampuni kutaongeza upatikanaji wa ajira kwa vijana na kukuza kipato cha wananchi na kuwawezesha wavuvi wadogo wadogo kuvua katika bahari ya kina kirefu. Hayo aliyaeleza wakati akizinduwa bodi ya Mamlaka ya Uvuvi, na kuchaguliwa kwa ndugu Omar Hassan Omar kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo. Wakati huo huo Mhe. Hamad alizinduwa Bodi ya wakurugenzi taasisi ya utafiti wa Mifugo na kuitaka bodi kufanya tafiti kwa kutumia teknologia za kisasa ili kuweza kupata taarifa kamili za wafugaji, ardhi, maji na maeneo ya kufungia kwani hii itapelekea thamani ya nyama na kututoa kwenye ufugaji duni ambao hauleti tija kwa wafugaji walio wengi. Pia Mhe. Hamad amesisitiza suala la elimu ya ufugaji lipewe kipaumbele kwani tunaelekea kwenye biashara zaidi hivyo taasisi hiyo inatarajiwa kufanya kazi kwa bidii na kuonesha mabadiliko kwa kuwawezesha wafugaji waweze kuengeza uzalishaji wa mifugo iliyo bora. Nae Mwenyekiti wa Bodi hiyo profesa Saleh Idirsa aliwaomba wajumbe kuwa tayari kutekeleza majukumu waliopewa kwani Taifa linawahitaji kuleta maendeleo ya Mifugo nchini. Aidha Mhe. Hamad pia alizindua Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Serekali wa huduma za Matrekta na zana za kilimo alieleza kuwa Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza mikakati ya mangeuzi ya kiuchumi na kijamii ina lengo la kupunguza umaskini na kuongeza pato la Taifa. Kutokana na hayo imeona kuna umuhimu wa kuazisha wakala utakaowezesha wananchi kutokana na utegemezi wa zana duni za kilimo na kukiwezesha kilimo kuwa endelevu na cha kibiashara na chenye kumpatia tija mkulima. Bodi hiyo itakayo kuwa na majukumu ya kutoa ushauri juu ya kutayarisha na kufanya mapitio ya Sera zinazohusiana na malengo ya wakala pamoja na kushauri juu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa wakala wa Serekali wa huduma za Matrekta. Bodi ilimteuwa ndugu Haroub S. Nassor kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo. Akitoa ufafanuzi Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi ndugu Juma Ali Juma alisema uzinduzi wa Bodi hizo ni ishara tosha kuwa Serekali ipo tayari kuhudumia wakulima, wafugaji na wavuvi na kuona sekta hizi zinasonga mbele kwa kuzalisha mazoa yaliyo bora na yatakayokubalika kimataifa.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii