MAKALA YA PWEZA.
Fahamu maisha ya Pweza jinsi ya kuvuliwa kwake pamoja na
faida zake zilizokuwemo katika kitoweo hicho chenye afya nyingi katika mwili wa
binadaamu.
Hakika kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu mtukufu wa
daraja alieumba bahari, ikiwa ni sehemu kubwa kati ya zile zilizoko juu ya
mgongo wa ardhi, kimaumbile ni sehemu ya maji chumvi iliyojaa neema kubwa
ikihusisha viumbe tofauti, miongoni mwao ni pamoja na wanyama, samaki, wadudu
na jamii ya mimea.
Eneo hili lililosheheni viumbe hai limekua ni makaazi ya mamilioni ya viumbe
zikiwemo aina tofauti zenye kushangaza na kustaajabisha kutokana na ukubwa wao
ama namna ya maumbile yao mfano wanyama kama nyangumi.
Pweza ni kiumbe kilicho katika kundi la wanyama waishio
baharini, ingawaje watu wengi humjumuisha katika kundi la samaki ikiwa ni
kitoweo adhimu kinachopendwa na jamii za watu wa pwani.
Katika Makala hii, mtaalam kutoka Idara ya maendeleo na
Uvuvi Zanzibar Buriyani Musa Hassan anachambua mazingira anayoishi Pweza na
faida zake kwa afya ya binaadam.
Anasema Pweza ni Kiumbe wa baharini ambae ana kichwa
kinachounganika moja kwa moja na mikia minane 8 aidha anasema kuna zaidi ya
aina mia moja 100 za pweza
zinazopatikana kote ingawaje hapa Zanzibar kuna aina tatu kuu za Pweza.
Anasema maisha ya Pweza ni ya kujitenga wakiwa na uwezo wa
kujigeuzageuza rangi kulingana na mazingira yaliyowazunguka, KWANI Pweza huweza
kujibadilisha rangi ili aweze kujilinda na maadui zake au aweze kuwinda chakula
chake kwa urahisi (anasema Buriyani).
Aidha anasema Pweza ana tabia ya kumwaga wino kutoka katika
kifuko maalum pale anapobaini kukabiliwa na mazingira hatari, hufanya hivyo ili
aweze kuondoka katika eneo la hatari bila ya adui yake kutambua.
Akifafanua Chakula cha Pweza, Anasema aina hii ya Samaki
hupendelea zaidi kula chakula cha asili kama vile konokono bahari pamoja na
samaki wadogo wadogo.
Pia Pweza hupendelea sana kutafuta chakula chao katika
nyakati za usiku ndio wakati wanaoweza kuona vitu kwa umakini mkubwa.
Kwa Upande wa Uzazi wa Pweza, viumbe hivi hupatikana zaidi
katika maji yaliyokaribu na mwambao na mara nyingi hupendelea sana kuishi
katika mazingira tofauti kama vile katika mapango, nyufa za majabali au mwamba
na huweza kujificha kwa urahisi dhidi ya maadui zake na pia kumuwezesha kutaga
na kulinda mayai yake.
Kwa upande wa Pweza dume hutoa mbegu za kiume kwa kutumia
sehemu maalum katika ncha moja ya mkia wake na hatimae husafirishwa hadi kwenye
kifuko cha mayai cha pweza jike.
Anasimulia Buriyani.
Anasema baada ya mayai kurutubishwa Pweza jike huyaweka
mayai hayo katika eneo lililo salama na kuyalinda, sambamba na kuyatunza hadi
yanapoanguliwa.
Anasema Pweza ana uwezo wa kutaga mayai kati ya laki mbili
hadi laki nne kwa mkupuo mmoja hvyo ni muhimu sana kuvua pweza aliepea, kwani
Pweza huishi kwa kipindi cha hadi miaka mitano na ni maalum kufa baada ya mayai
yake kuanguliwa, lakini Pweza dume yeye
hufa muda mfupi tu baada ya kuyarutubisha mayai, Anafafanua.
Maadui wa Pweza, Katika mazingira ya maisha yake ya
baharini, pweza ana maadui wengi ambao humuwinda kwa ajili ya chakula miongoni
mwao ni pamoja na ndege, samaki aina ya mkunga, nyangumi pamoja na binaadamu,
hvyo mtaalam anasema kua binaadam ndie adui mkubwa wa Pweza kwani ana uwezo wa
kumvua kupitia mbinu tofauti.
Wakati mtaalam wa pweza akimchambua mnyama huyu kisayansi
kwani mvuvi maarufu wa siku nyingi kutoka ukanda wa kusini Mashariki Abdalla
masangu wenye umri wa miaka 59 mkaazi wa
kumbini makunduchi anamuelezea Samaki huyu kiuhalisia.
Mzee masangu anasema kila kiumbe duniani iwe kikubwa au
kidogo kimejaaliwa kuwa na silaha ya kujilinda kutokana na maadui zake, Pweza
nao wakiwa ni viumbe wanaowindwa zaidi na binaadamu, Mola amewabariki na silaha
za kujilinda.
Amesema Pweza amejaaliwa kua na aina Fulani ya wino mweusi
ambapo hutumia kwa ajili ya kujilinda pale anapokua majini anasema kua pale
anapomuona binaadamu humwaga wino huo ili kudanganya binaadamu asimuone
sambamba na kuondoka katika eneo hilo haraka na kukimbilia kwengineko.
Hata hivyo anasema kua hakika ni kazi kubwa ya kitaalamu
kubaini nyumba ya pweza akifafanua kua ni shimo lenye tundu mbili, ikiwemo ile
ya kuingilia na kutokea.
Miongoni mwa mambo ya msingi na ya kuzingatia wakati wa
kuvua Pweza ni kwa mvuvi kutofanya papara na kuvua kwa umakini mkubwa kwani
anapaswa kuondosha jiwe moja na kuweka kando, na baadae kuingiza mti maalum kwa
ajili ya kuchokolea ndani ta koma hadi kumgusa pweza aliomo ndani na kubainisha
kuwa kero linapozidi pweza huyo hulazimika kutoka nje na kuivaranga mikono ya
mvuvi kupitia mikonyo yake kuelekea juu kwapani kwa mvuvi.
Hata hivyo mbali ya yote hayo matumizi ya kawaida ya pweza
kwa ajili ya mchuzi, hususan wa nazi pale unapompata kwa mseto wa choroko,
vilevile Pweza ni tiba kubwa kwa akina mama wanapojifungua husaidia utoaji wa
maziwa kwa wingi na kwa urahisi.
Aidha kuna imani iliyothibiti hususan kwa akina baba wa
maeneo ya pwani kua pweza ni mjarabu kwani anaongeza uwezo wa nguvu za kiume na
kuwa makini zaidi katika tendo la kujamiiana.
Kwa upande wa mtoto mdogo akiwa hapati choo kidogo huchemshiwa
pweza mkavu na kunyweshwa mchuzi wake lakini hata akibainika kuwa na uwezo
mdogo wa nguvu za kiume pia hupewa pweza.
Wakati mahitaji ya samaki yakiongezeka mjini na vijijini
kutokana na kuimarika kwa sekta ya utalii nchini, hali hiyo inakwenda sambamba
na kupanda kwa bei ya Pweza ambapo hivi sasa kilo moja ya Samaki huyo adhimu
inauzwa hadi shilingi elf 7,000/.
Mwandishi Salama Ramadhan
Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi
Maoni
Chapisha Maoni