MAKALA YA PWEZA.

Fahamu maisha ya Pweza jinsi ya kuvuliwa kwake pamoja na faida zake zilizokuwemo katika kitoweo hicho chenye afya nyingi katika mwili wa binadaamu.
Hakika kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu mtukufu wa daraja alieumba bahari, ikiwa ni sehemu kubwa kati ya zile zilizoko juu ya mgongo wa ardhi, kimaumbile ni sehemu ya maji chumvi iliyojaa neema kubwa ikihusisha viumbe tofauti, miongoni mwao ni pamoja na wanyama, samaki, wadudu na jamii ya mimea.
Eneo hili lililosheheni viumbe  hai limekua ni makaazi ya mamilioni ya viumbe zikiwemo aina tofauti zenye kushangaza na kustaajabisha kutokana na ukubwa wao ama namna ya maumbile yao mfano wanyama kama nyangumi.
Pweza ni kiumbe kilicho katika kundi la wanyama waishio baharini, ingawaje watu wengi humjumuisha katika kundi la samaki ikiwa ni kitoweo adhimu kinachopendwa na jamii za watu wa pwani.
Katika Makala hii, mtaalam kutoka Idara ya maendeleo na Uvuvi Zanzibar Buriyani Musa Hassan anachambua mazingira anayoishi Pweza na faida zake kwa afya ya binaadam.
Anasema Pweza ni Kiumbe wa baharini ambae ana kichwa kinachounganika moja kwa moja na mikia minane 8 aidha anasema kuna zaidi ya aina  mia moja 100 za pweza zinazopatikana kote ingawaje hapa Zanzibar kuna aina tatu kuu za Pweza.
Anasema maisha ya Pweza ni ya kujitenga wakiwa na uwezo wa kujigeuzageuza rangi kulingana na mazingira yaliyowazunguka, KWANI Pweza huweza kujibadilisha rangi ili aweze kujilinda na maadui zake au aweze kuwinda chakula chake kwa urahisi (anasema Buriyani).
Aidha anasema Pweza ana tabia ya kumwaga wino kutoka katika kifuko maalum pale anapobaini kukabiliwa na mazingira hatari, hufanya hivyo ili aweze kuondoka katika eneo la hatari bila ya  adui yake kutambua.
Akifafanua Chakula cha Pweza, Anasema aina hii ya Samaki hupendelea zaidi kula chakula cha asili kama vile konokono bahari pamoja na samaki wadogo wadogo.
Pia Pweza hupendelea sana kutafuta chakula chao katika nyakati za usiku ndio wakati wanaoweza kuona vitu kwa umakini mkubwa.
Kwa Upande wa Uzazi wa Pweza, viumbe hivi hupatikana zaidi katika maji yaliyokaribu na mwambao na mara nyingi hupendelea sana kuishi katika mazingira tofauti kama vile katika mapango, nyufa za majabali au mwamba na huweza kujificha kwa urahisi dhidi ya maadui zake na pia kumuwezesha kutaga na kulinda mayai yake.
Kwa upande wa Pweza dume hutoa mbegu za kiume kwa kutumia sehemu maalum katika ncha moja ya mkia wake na hatimae husafirishwa hadi kwenye kifuko cha mayai cha pweza  jike. Anasimulia Buriyani.
Anasema baada ya mayai kurutubishwa Pweza jike huyaweka mayai hayo katika eneo lililo salama na kuyalinda, sambamba na kuyatunza hadi yanapoanguliwa.
Anasema Pweza ana uwezo wa kutaga mayai kati ya laki mbili hadi laki nne kwa mkupuo mmoja hvyo ni muhimu sana kuvua pweza aliepea, kwani Pweza huishi kwa kipindi cha hadi miaka mitano na ni maalum kufa baada ya mayai yake kuanguliwa,  lakini Pweza dume yeye hufa muda mfupi tu baada ya kuyarutubisha mayai, Anafafanua.
Maadui wa Pweza, Katika mazingira ya maisha yake ya baharini, pweza ana maadui wengi ambao humuwinda kwa ajili ya chakula miongoni mwao ni pamoja na ndege, samaki aina ya mkunga, nyangumi pamoja na binaadamu, hvyo mtaalam anasema kua binaadam ndie adui mkubwa wa Pweza kwani ana uwezo wa kumvua kupitia mbinu tofauti.
Wakati mtaalam wa pweza akimchambua mnyama huyu kisayansi kwani mvuvi maarufu wa siku nyingi kutoka ukanda wa kusini Mashariki Abdalla masangu wenye umri wa miaka 59  mkaazi wa kumbini makunduchi anamuelezea Samaki huyu kiuhalisia.
Mzee masangu anasema kila kiumbe duniani iwe kikubwa au kidogo kimejaaliwa kuwa na silaha ya kujilinda kutokana na maadui zake, Pweza nao wakiwa ni viumbe wanaowindwa zaidi na binaadamu, Mola amewabariki na silaha za kujilinda.
Amesema Pweza amejaaliwa kua na aina Fulani ya wino mweusi ambapo hutumia kwa ajili ya kujilinda pale anapokua majini anasema kua pale anapomuona binaadamu humwaga wino huo ili kudanganya binaadamu asimuone sambamba na kuondoka katika eneo hilo haraka na kukimbilia kwengineko.
Hata hivyo anasema kua hakika ni kazi kubwa ya kitaalamu kubaini nyumba ya pweza akifafanua kua ni shimo lenye tundu mbili, ikiwemo ile ya kuingilia na kutokea.
Miongoni mwa mambo ya msingi na ya kuzingatia wakati wa kuvua Pweza ni kwa mvuvi kutofanya papara na kuvua kwa umakini mkubwa kwani anapaswa kuondosha jiwe moja na kuweka kando, na baadae kuingiza mti maalum kwa ajili ya kuchokolea ndani ta koma hadi kumgusa pweza aliomo ndani na kubainisha kuwa kero linapozidi pweza huyo hulazimika kutoka nje na kuivaranga mikono ya mvuvi kupitia mikonyo yake kuelekea juu kwapani kwa mvuvi.
Hata hivyo mbali ya yote hayo matumizi ya kawaida ya pweza kwa ajili ya mchuzi, hususan wa nazi pale unapompata kwa mseto wa choroko, vilevile Pweza ni tiba kubwa kwa akina mama wanapojifungua husaidia utoaji wa maziwa kwa wingi na kwa urahisi.
Aidha kuna imani iliyothibiti hususan kwa akina baba wa maeneo ya pwani kua pweza ni mjarabu kwani anaongeza uwezo wa nguvu za kiume na kuwa makini zaidi katika tendo la kujamiiana.
Kwa upande wa mtoto   mdogo akiwa hapati choo kidogo huchemshiwa pweza mkavu na kunyweshwa mchuzi wake lakini hata akibainika kuwa na uwezo mdogo wa nguvu za kiume pia hupewa pweza.

Wakati mahitaji ya samaki yakiongezeka mjini na vijijini kutokana na kuimarika kwa sekta ya utalii nchini, hali hiyo inakwenda sambamba na kupanda kwa bei ya Pweza ambapo hivi sasa kilo moja ya Samaki huyo adhimu inauzwa hadi shilingi elf 7,000/.

Mwandishi Salama Ramadhan 
Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii