
MAKALA YA PWEZA . Fahamu maisha ya Pweza jinsi ya kuvuliwa kwake pamoja na faida zake zilizokuwemo katika kitoweo hicho chenye afya nyingi katika mwili wa binadaamu. Hakika kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu mtukufu wa daraja alieumba bahari, ikiwa ni sehemu kubwa kati ya zile zilizoko juu ya mgongo wa ardhi, kimaumbile ni sehemu ya maji chumvi iliyojaa neema kubwa ikihusisha viumbe tofauti, miongoni mwao ni pamoja na wanyama, samaki, wadudu na jamii ya mimea. Eneo hili lililosheheni viumbe hai limekua ni makaazi ya mamilioni ya viumbe zikiwemo aina tofauti zenye kushangaza na kustaajabisha kutokana na ukubwa wao ama namna ya maumbile yao mfano wanyama kama nyangumi. Pweza ni kiumbe kilicho katika kundi la wanyama waishio baharini, ingawaje watu wengi humjumuisha katika kundi la samaki ikiwa ni kitoweo adhimu kinachopendwa na jamii za watu wa pwani. Katika Makala hii, mtaalam kutoka Idara ya maendeleo na Uvuvi Zanzibar Buriyani Musa Hassan anachambua mazing...